Mshukiwa wa kughushi cheti afikishwa mahakamani

Mshukiwa huyo Victor Ochieng Odhiambo alikamatwa katika uwanja wa ndege wa JKIA akirejea nchini kutoka Korea Kusini.

Marion Bosire
1 Min Read

Jamaa kwa jina Victor Ochieng Odhiambo leo alifikishwa katika mahakama ya Milimani jijini Nairobi kwa ajili ya kula kiapo, katika kesi inayomkabili ya kughushi cheti.

Odhiambo alikanusha mashtaka dhidi yake na kuachiliwa kwa dhamana ya shilingi laki 3 pesa taslimu au dhamana ya shilingi laki 5 na mdhamini mmoja wa kiasi sawa na hicho.

Mshukiwa huyo ambaye kesi yake itatajwa Aprili 2, 2026, kikao kitakachotumiwa pia kujiandaa kwa ajili ya kusikilizwa kwa suala hilo, alikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, JKIA.

Odhiambo alikuwa akirejea nchini kutoka Korea Kusini alipokamatwa na maafisa wa idara ya uhamiaji waliokuwa wamepashwa habari kumhusu na kupelekwa katika kituo cha polisi cha Muthaiga.

Uchunguzi unaonyesha kwamba Odhiambo amekuwa akisakwa kwa makosa ya kughushi cheti kinyume cha kifungu nambari 345 na 349 cha kanuni za adhabu.

Alighushi cheti cha shahada ya uhandisi wa kielektroniki ambacho alitumia kupata ajira katika kampuni ya serikali ya Kenya Pipeline kama afisa mkuu wa teknolojia.

Cheti hicho ghushi kina nambari 296168 na kinaripotiwa kutolewa tarehe 19 mwezi Disemba mwaka 2008.

Share This Article