Wakazi wa eneo bunge la Mwala katika kaunti ya Machakos wanazidi kunufaika na mradi wa maji kwenye mto Miu unaotekelezwa na jamii kwa kusudi la kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, almaarufu FLLoCA.
Tangu kuanzishwa kwa mradi huo unaopigwa jeki na Hazina Kuu, eneo hilo limeshuhudia mabadiliko ya kupigiwa mfano.
Mabadiliko hayo ni pamoja na kuimarishwa kwa shughuli za kilimo kupitia unyunyiziaji mashamba maji, upatikanaji wa maji ya matumizi ya nyumbani na mifugo pamoja na upanzi wa miti.
Peter Odhengo ni mshirikishi wa mradi wa FLLoCA. Amedokeza kuwa wakazi wapatao 4,000 wananufaika moja kwa moja na mradi huo ulioazishwa miaka miwili iliyopita.
Kwenye mradi huo, maji yamezuiwa upande mmoja kwa kujenga ukuta kwa lengo la kuhakikisha upatikanaji wa maji nyakati zote.

“Mradi huu unawanufaisha kina mama, wakulima na wale wanaoishi na ulemavu. Maji kutoka kwa mto huu husafishwa na kutumiwa kwa shughuli za nyumbani,” alisema Odhengo.
Aliongeza kuwa tangu kuanzishwa kwake, mradi huo umefanikisha ufadhili wa moja kwa moja wa jamii kupitia serikali za kaunti, hatua inayowezesha jamii kubuni na kutafuta suluhisho la changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.
“Huku kiwango cha joto kikizidi kuongezeka, jamii ndio huwa inaumia zaidi kutokanana ukame wa muda mrefu na mafuriko, jinsi ilivyoshuhudiwa miezi kadhaa iliyopita,” alisema Odhengo.

Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi wa kaunti ya Machakos Onesmus Muia amesema serikali ya kaunti hiyo inajizatiti kuhakikisha wakazi zaidi wanaendelea kufurahia matunda ya mradi huo.
“Sisi kama kaunti, tunashirikiana kwa karibu na mradi huu wa FLLoCA, kuhakikisha wakazi wetu hawaathiriwi na mabadiliko ya tabianchi,” alisema Muia.
Robert Mutiso ni mkazi wa kijiji cha Ulaani, eneo bunge la Mwala. Anaungama kuwa mradi huo umesababisha utoshelevu wa chakula, upatikanaji wa maji na kufanikisha upanzi wa miti.

Mradi wa FLLoCA umepata ufadhili zaidi wa shilingi bilioni 3.9 kutoka Benki ya Dunia kutokana na ongezeko la miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kote nchini.