Mikutano Miwili: Dirisha muhimu kwa nchi za nje kujifunza maendeleo ya China

Wajumbe kutoka kote nchini hukusanyika Beijing kushiriki moja ya matukio muhimu zaidi kwenye kalenda ya kisiasa ya China.

KBC Digital News
6 Min Read
Maelezo ya picha: Waandishi mbalimbali wa habari wakisikiliza viongozi wa Mkoa wa Anhui wakipitia ripoti ya kazi ya serikali, na rasimu ya mpango wa 15 wa miaka mitano pembeni ya Mkutano wa Nne wa Bunge la 14 la Umma la China (NPC) hapa Beijing.

Na CGTN Kiswahili

“Mikutano Miwili”, yaani Mkutano wa Bunge la Umma la China na Mkutano wa Baraza la Mashauriano ya Kisiasa la China, ambayo hufanyika kila mwanzoni mwa mwaka hapa China, imeanza rasmi Machi 4 na kuendelea hadi Machi 11. Kawaida katika kipindi hiki maelfu ya wajumbe kutoka kote nchini hukusanyika Beijing kushiriki moja ya matukio muhimu zaidi kwenye kalenda ya kisiasa ya China.

Kwanini “Mikutano Miwili” ya mwaka huu ni muhimu sana?

Mwaka huu ni muhimu sana kwa sababu serikali sio tu kwamba ina ajenda ya kutangaza malengo yake ya kiuchumi ya kila mwaka bali pia imechapisha Mpango wa 15 wa Miaka Mitano, unaoelezea malengo ya sera ya 2026-2030. Mambo muhimu ya mpango huo ambayo ni pamoja na kuongeza mahitaji ya ndani na kujenga uwezo wa China katika teknolojia za kisasa, hasa muunganisho wa nyuklia, teknolojia ya quantum na Akili Mnemba, yalitolewa mwaka jana, baada ya kufanywa rasimu na maafisa wakuu wa CCP.

Aidha mikutano hii huangalia lengo la ukuaji wa mwaka. Takwimu, zilizopangwa kusomwa katika ripoti ya kazi ya serikali mwanzoni mwa kikao cha bunge, huwa ni miongoni mwa mada zinazosubiriwa kwa hamu sana kila mwaka. Sambamba na hayo ripoti ya kazi ya serikali huwa inaangazia viashiria vingine muhimu vya kiuchumi, ikiwa ni pamoja na uwiano wa nakisi ya Pato la Taifa na lengo la mfumuko wa bei.

Wakati inapofanyika mikutano hii miwili ya kila mwaka, pembeni pia huwa vinafanyika vikao vingine mfululizo vya kamati za chama na serikali za mikoa mbalimbali, pamoja na vikao vya makundi mbalimbali, ambavyo mbali na mambo mengine pia hutumika kuwasilisha ripoti zao za kazi. Ripoti hizo hutaja mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita tangu mikutano miwili ifanyike na kuangalia mafanikio zaidi katika mwaka unaofuata.

Ripoti za kazi za “Mikutano Miwili” zinaonesha Anhui imepata matokeo ya kushangaza kwenye teknolojia

Kama mwaka jana, na mwaka huu pia nimebahatika kuhudhuria kikao cha manaibu wa ujumbe kutoka Mkoa wa Anhui kilichofanyika Machi 6, pembeni ya Mkutano wa Nne wa Bunge la 14 la Umma la China (NPC) hapa Beijing. Ikumbukwe kwamba kabla ya kikao hiki, mwanzoni mwa Februari Mkoa wa Anhui ulifanya mikutano yake miwili ya ngazi ya jimbo, ambapo wajumbe na manaibu wa Baraza la Mashauriano ya Kisiasa la China (CPPCC) na Bunge la Umma la Mkoa huo kutoka sekta tofauti walitoa mawazo na mapendekezo yao kuhusu maendeleo ya kiuchumi, uvumbuzi wa kiteknolojia, na ustawi wa watu wa mkoa huo.

Katika kikao cha mkoa wa Anhui kilichofanyika Beijing, shughuli kubwa ilyofanyika ilikuwa ni kupitia ripoti ya kazi ya serikali, pamoja na kupitia rasimu ya mpango wa 15 wa miaka mitano. Viongozi wa sekta mbalimbali zikiwemo za sayansi na teknolojia, kilimo, utamaduni, masuala ya demokrasia, taasisi za utafiti na nyinginezo zilitoa wawakilishi wao ambao waliwasilisha ripoti za kazi zao. Cha kutia moyo ni kwamba takwimu zinaonesha kila mwaka wanaporudi kwenye vikao hivi, mkoa wa Anhui unafanya vizuri zaidi kwa kupata matokeo ya kushangaza kwenye nyanja mbalimbali ikilinganishwa na mwaka wa nyuma yake.

Mkoa wa Anhui wenye kiasi cha idadi ya watu wapatao milioni 61.2, kwa sasa unashuhudia mabadiliko makubwa, na hii ni kutokana na nguvu kubwa uliyonayo kwenye masuala ya uvumbuzi wa kiteknolojia hasa katika utengenezaji wa roboti za kisasa, uchunguzi wa anga za juu na maabara za kisasa kabisa. Na kwa mujibu wa manaibu wa baraza, ni kwamba mkoa huo unatarajia kuondoa changamoto zote za kiufundi na kuweza kuzalisha kwa wingi roboti.

Kutokana na maendeleo yake ya kasi ya teknolojia, wakaazi wa Hefei wanasema mji wao una majua mawili, moja lililopo juu angani na jingine jua bandia lililopo kwenye bustani ya viwanda nje ya mji huo, hasa kwasababu mji huo unafanya majaribio ya “Experimental Advanced Superconducting Tokamak” (EAST) ambao umepewa jina la “jua bandia” la China kutokana na mchakato wake wa kipekee wa muunganisho unaoiga ule wa jua.

Maelezo ya picha: Januari 15, 2026, katika Ukumbi wa Udhibiti wa EAST wa Taasisi ya Fizikia ya Plasma, Chuo cha Sayansi cha China, huko Hefei, Anhui.

Mafanikio mengine wanayoendelea kujivunia watu wa mkoa wa Anhui ni kwamba mwaka huu ulitunukiwa heshima ya kuwa ukumbi mmoja wapo kati ya kumbi nne za China ambazo zimetoa jukwaa la kuandaa Tamasha la Sikukuu ya Mwaka Mpya wa Jadi wa China, lililoandaliwa na Shirika Kuu la Utangazaji la China (CMG). Ukitumia teknolojia zake za juu, mji wa Hefei uliandaa maonesho murua kabisa.

Kutokana na ushindani wa kimkakati na kutokuwa na uhakika duniani, Beijing itaendelea kusisitiza kujitegemea ndani ya nchi pamoja na ustahimilivu wa nje.

Kwa nini “Mikutano Miwili” ya China ni umuhimu kwa ulimwengu?

“Mikutano Miwili” ni dirisha muhimu kwa nchi za nje hasa za Afrika kujifunza kuhusu maendeleo ya sasa ya China, kuelewa mfumo wa kisiasa wa China na kutabiri njia yake ya maendeleo ya baadaye. Katika kipindi hiki, wageni wanaweza kujua ni mada gani nzito zinazojadiliwa hapa nchini, ni masuala gani wanayofuatilia zaidi viongozi wa China, ni malengo gani ya maendeleo yaliyowekwa, ni namna gani China inavyoingiliana na nchi nyingine, n.k.

Share This Article