Mwanasiasa Rose Mbithe na wanawe Chris Mulwa na Angela Mulwa wamekana mashtaka ya kumuua Dkt. Victoria Nthunya Mutiso.
Wengine waliokana mashtaka walipofikishwa mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu ya Milimani Alexander Muteti ni Konstebo wa Polisi Elijah Kimutai na Maritim Kimutai.
Kesi ya kusikiliza ikiwa washukiwa wote watano watapewa dhamana au la imepangwa kufanyika Oktoba 6.
Wakati wa kesi hiyo, mawakili waliokuwa wakimwakilisha Mbithe na wanawe wawili waliomba kujiondoa kwenye kesi hiyo kwa madai ya washtakiwa kutozingatia ushauri wao wa kisheria.
Mawakili waliojiondoa kwenye kesi hiyo ni Cliff Ombata, Danstan Omari na Sam Nyaberi.
Dkt. Mutiso aliuawa na watu wasiojulikana katika eneo la Upper Hill jijini Nairobi Julai 29 mwaka huu.
Uchunguzi wa DCI uliashiria kuwa Mbithe na wanawe walikula njama na maafisa hao wa polisi kumuua Dkt. Mutiso mwishoni mwa mwezi Julai.
Uchunguzi wa DCI ukibaini kuwa kiini cha mauaji hayo ni mzozo wa ardhi iliyopo katika eneo la Mlolongo, kaunti ya Machakos.
Mbithe pia anatuhumiwa kuhusika katika mauaji ya wakili Mathew Kyalo Mbobu yanayohusiana na ardhi hiyo.