Mashirika sita ya kitaifa yanayowakilisha wanablogu, wanahabari, mawakili, wataalamu wa afya na watetezi wa haki za binadamu, yametoa taarifa ya pamoja kulaani ukiukaji wa haki za binadamu unaoendelea nchini Kenya.
Taarifa hiyo inaangazia hitaji la haraka la hatua madhubuti za kiutendaji ili kutatua janga lililotokana na kupingwa kwa Mswada wa Fedha 2024.
Kulingana na taarifa hiyo, kufikia jana Jumapili usiku, watu 24 walikuwa wamedaiwa kuuawa na polisi na angalau 361 kuripotiwa kujeruhiwa. Miongoni mwa waliouawa ni mtoto wa miaka kumi na mbili, Kennedy Onyango.
Aidha, kumekuwa na watu 627 waliokamatwa na 32 waliotekwa nyara, wengi wao wakishikiliwa bila mashtaka rasmi au kupata uwakilishi wa kisheria.
Wahudumu wa afya wamekumbana na changamoto kubwa, ikiwa ni pamoja na kukamatwa na wizi wa orodha za wagonjwa kutoka vituo vya dharura vya rununu vinavyowahudumia waliojeruhiwa.
Mawakili wamezuiwa kupata wateja wao na kutishwa. Baadhi ya wanahabari waliokuwa wakifuatilia maandamano wamepoteza vifaa vyao na wamekamatwa na kupigwa hadharani. Wafanyakazi wanaosaidia kutoa msaada wa kisheria na matibabu pia wamekumbwa na unyanyasaji.
Mashirika hayo yanakubali tangazo la Ikulu la mazungumzo ya sekta mbalimbali ili kushughulikia masuala ya sera yaliyoibuliwa na vuguvugu la maandamano la Vijana kwa Kenya (Gen Z).
Hata hivyo, wanahoji kwamba masuala mengi yanahitaji hatua madhubuti za kiutendaji badala ya mijadala ya muda mrefu.
Vijana wanadai kuchukuliwa hatua dhidi ya ufisadi, kupunguzwa kwa baraza la mawaziri lililozidi, uwekezaji katika huduma muhimu, uwajibikaji kwa wale waliowafyatulia risasi waandamanaji wasio na silaha, kuachiliwa kwa watu waliokamatwa kiholela na kukomeshwa kwa mauaji ya kikatili.
Mashirika hayo yanahimiza serikali kuu na serikali za kaunti kusikiliza na kufanyia kazi matakwa ya Gen Z, ambao wanawakilisha Wakenya.
Wito unaoelekezwa kwa serikali ni kuheshimu mamlaka yao na kusitisha unyanyasaji wa wafanyakazi na kuvuruga huduma za umma. Pia wanavyotaka vikosi vya usalama vikome kushambulia vituo vya kutoa matibabu ya dharura na kuhakikisha usalama wa wahudumu wa afya wakati wa maandamano yaliyopangwa.
Serikali inahimizwa kugharamikia gharama za matibabu ya waliojeruhiwa na kutimiza wajibu wa kikatiba wa kutoa huduma za afya kwa wote, wakiwemo waandamanaji.
Huduma ya Kitaifa ya Polisi inaombwa kusitisha kufanyia waandamanaji uhalifu na kuacha kutumia maafisa wasio na sare rasmi na magari yasiyo na alama za wazi. Polisi na wanajeshi wanakumbushwa kufanya kazi ndani ya mifumo ya katiba na haki za binadamu wakati wa maandamano.
Chama cha Wanasheria nchini, LSK, Tume ya Kutetea Haki za Binadamu, KHRC, shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International Kenya na Chama cha Wanahabari nchini, KUJ ni miongoni mwa taasisi zilizotia saini taarifa hiyo.