Mahakama yampata Mackenzie na mashtaka ya kujibu

Tom Mathinji
1 Min Read
Mhubiri tata Paul Mackenzie apatikana na kesi ya kujibu.

Mahakama ya Shanzu imempata mhubiri tata Paul Mackenzie na washtakiwa wenza 95 na kesi ya kujibu, baada ya kuhusishwa na maafa katika shamba la Shakahola kaunti ya Kilifi.

Kulingana na mahakama hiyo, washukiwa hao wamepatikana na makosa ya kushirki uhalifu wa kupangwa na itikadi kali zinazohusishwa na vifo vya watu 450 katika msitu wa Shakahola.

Mahakama hiyo ilidokeza kuwa upande wa mashtaka uliwasilisha ushahidi wa kutosha dhidi ya washukiwa wote, na sasa wanakabiliwa na makosa ya kujibu.

Upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi 96, wakiwemo manusura, wataalam, wachunguzi na kuwasilisha vifa 500 kama sehemu ya ushahidi.

Wafuasi wa mhubiri huyo tata wanadaiwa kuhadaiwa kuwa imani potovu, iliyojumuisha kususia chakula hadi kufa kama njia ya wokovu, hatua iliyosababisha mauti ya halaiki katika msitu wa Shakahola.

Mackenzie, mke wake Rhoda Mumbua Maweu na washtakiwa wenza, hata hivyo walikanusha mashtaka kadhaa yaliyohusiana na ugaidi, ikiwa ni pamoja na kufanikisha shughuli za kigaidi na kueneza itikadi kali na hivyo kuhatarisha maisha.

Mackenzie na washtakiwa wenza pia wanakabiliwa na mashtaka tofauti ya mauaji ya watu 52 katika eneo la Kwa Binzaro, Malindi.

Share This Article