Kaunti ya Nairobi ndio iliyoathiriwa zaidi kutokana na vifo vilivyosababishwa na mafuriko yaliyoshuhudiwa nchini Ijumaa iliyopita, Machi 6, 2026.
Jumla ya watu 49 wamethibitishwa kufariki kutokana na mafuriko hayo kote nchini.
Akiwahutubia wanahabari jijini Mombasa, msemaji wa serikali Isaac Mwaura amesema jumla ya watu 27 wamethibitishwa kufariki katika kaunti ya Nairobi pekee.
Watu 11 wameripotiwa kufariki katika eneo la Mashariki, 5 katika eneo la Bonde la Ufa huku maeneo ya Pwani na Nyanza yakiripoti kifo cha mtu mmoja kila eneo.
Kulingana na Mwaura, watu 4 bado hawajulikani waliko huku wengine 4 wakiendelea kupokea matibabu hospitalini kutokana na majeraha.
Familia zaidi ya 9,000 zimepoteza makazi huku Nairobi ikiongoza kwa familia 5,260 ikifuatwa na Bonde la Ufa (2,538, eneo la Kati (434), Nyanza (415), Pwani (282), eneo la Mashariki familia 58 huku familia 46 zikipoteza makazi katika eneo la Magharibi.
Kaunti zilizoathiriwa na hali hiyo ni Tana River, Kilifi, Kwale, Taita Taveta, Narok, Baringo, Nandi, Makueni, Kitui na Tharaka Nithi. Zingine ni Marsabit, Meru, Kiambu, Kisumu, Kisii, Homa Bay, Migori, Wajir na Nairobi.
Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa nchini inasema mvua kubwa inaweza kunyesha katika maeneo ya nyanda za juu mashariki na magharibi mwa Bonde la Ufa, eneo la Ziwa Victoria, Bonde la Ufa, nyanda za chini upande wa kusini na mashariki na Pwani Kusini.
Wakenya wametakiwa kuendelea kuchukua tahadhari wakati huu wa msimu wa mvua na kuzingatia ushauri unaotolewa na mamlaka husika.