Waziri wa mambo ya ndani, Kipchumba Murkomen, amewataka madereva kuwa waangalifu barabarani na kuzingatia kanuni na sheria za usalama wa barabarani.
Alikuwa akizungumza katika Kaunti ya Mombasa baada ya kumtembelea mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya bandari ya Kenya, William Ruto, ambaye alipata ajali mbaya ya barabarani katika Kaunti ya Taita Taveta juzi jioni pamoja na familia yake.
Murkomen alihimiza idara ya polisi wa trafiki pamoja na Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama Barabarani, NTSA, kushirikiana na umma ili kuhakikisha barabara zinakuwa salama.
Murkomen alithibitisha kuwa Kapteni William Ruto hayuko hatarini kufuatia ajali hiyo mbaya ya barabarani katika Kaunti ya Taita Taveta iliyosababisha kifo cha binti yake.
Familia hiyo ilikuwa ikisafiri kuelekea Arusha, nchini Tanzania kwa likizo ya Pasaka wakati gari walilokuwa wakisafiria liligonga trela iliyokuwa imesimama.
Murkomen alisema familia hiyo inaendelea kuimarika vyema.
Haya yanajiri wakati ambapo ajali nyingi za barabarani zinashuhudiwa hasa wakati huu wa shughuli nyingi kutokana na sherehe za pasaka.
Yanafuatia pia ajali mbili mbaya za barabarani ambazo serikali ililazimika kuingilia na kusaidia waathiriwa, moja huko Webuye ambapo watu zaidi ya 17 walifariki na nyingine huko Nyeri ambapo watu 16 walifariki.
Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama Barabarani, NTSA ilianzisha msako wa barabarani kwa ushirikiano na asasi husika kama polisi ili kuhakikisha usalama wa wakenya barabarani wanaposherehekea pasaka.