Maafisa 215 wa polisi ambao ni sehemu ya kikosi cha maafisa wa usalama wa kimataifa wanaorejesha hali ya utulivu nchini Haiti, wamerejea nchini.
Akiwapokea maafisa hao, Katibu katika Wizara ya Usalama wa Taifa Dkt. Raymond Omollo amesema maafisa hao walikuwa miongoni mwa maafisa waliotumwa nchini Haiti mwaka 2023 kurejesha utulivu nchini humo.
Aidha, walipelekwa nchini humo ili kupiga jeki Huduma ya Taifa ya Polisi ya Haiti kudumisha amani katika maeneo yaliyokumbwa na ghasia.
Huduma zao zilikuwa sehemu ya juhudi zinazotekelezwa na Kenya katika kikosi cha kimataifa kinachoongozwa na Umoja wa Mataifa kulinda raia, miundombinu na kuimarisha uwezo wa maafisa wa usalama wa taifa hilo.
Walipowasili nchini, maafisa hao walilakiwa na Katibu Omollo na Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja miongoni mwa maafisa wengine.