Naibu Rais Kithure Kindiki amewahimiza Wakenya ambao hawajasajiliwa kujitokeza kwa wingi na kujiandikisha kama wapiga kura kabla ya muda wa usajili kufungwa.
Akizungumza nyumbani kwake huko Irunduni, Kaunti ya Tharaka Nithi, Kindiki alisema watakaokosa kujisajili, watapoteza uwezo wa kuchagua viongozi wanaowataka katika uchaguzi ujao.
Kiongozi huyo aliandalia wakazi sherehe ya pasaka nyumbani ambapo aliwasisitizia kwamba bila kura, watapiga kelele tu lakini hawatakuwa na haki ya kupiga kura.
Wakazi hao wenye furaha walipatiwa taarifa kuhusu miradi mikubwa ya maendeleo ambayo serikali inaendeleza katika kaunti hiyo na kote nchini.
Kindiki aliwasihi Wakenya kutoshawishiwa na wale wanaotaka kuwagawanya kwa misingi ya kisiasa, akihimiza upendo kati ya wakenya na kwa nchi yao.
Profesa Kindiki aliwahakikishia wakazi kwamba watanufaika na ajenda pana ya maendeleo ya serikali inayolenga barabara za lami kwa kila kaunti, kusambaza umeme kwa maelfu ya nyumba, ujenzi wa masoko ya kisasa, miradi ya maji miongoni mwa mingine.
Naibu Rais alisisitiza kuwa hakuna sehemu ya nchi itakayobaguliwa wakati serikali ikiendeleza miradi ya maendeleo inayolenga kuboresha maisha ya Wakenya wote.
“Tunaendeleza kila sehemu ya nchi kwa sababu si sahihi sehemu moja ya nchi kuendelea na nyingine kubaki nyuma. Kila sehemu ya nchi hii itaendelezwa,” alihakikishia.
Mapema jana, Naibu Rais alihudhuria ibada ya madhehebu mbalimbali kwa heshima ya aliyekuwa Mbunge wa Ol Kalou, marehemu David Kiaraho, nyumbani kwake katika kijiji cha Gacwe, Kaunti ya Nyandarua.