Kampuni ya Taifa Gas yapanua operesheni zake nchini Tanzania

Tom Mathinji
1 Min Read
Taifa Gas yapanua operesheni zake Tanzania.

Kampuni ya Taifa Gas Tanzania Limited, inayomilikiwa na mfanyabiashara Rostam Aziz, imetia saini makubaliano ya kununua kampuni ya Orca Energy Group Inc., na kuleta taswira mpya katika sekta ya Nishati nchini Tanzania.

Mnamo Aprili 13, 2026, tangazo lilitolewa kwamba Taifa Gas itanunua asilimia 49 ya shirika la PAE PanAfrican Energy Corporation (PAEM), huku kampuni ya Amber Energy Investment L.L.C-FZ , ikinunua asilimia 51 iliyosalia.

Makubaliano hayo yanahusu kuuza asilimia 100 ya biashara ya Orca, huku faida zote zikielekezwa kwenye mradi wa gesi wa Songo Songo, ambao ni chanzo muhimu cha gesi inayotumiwa kuzalisha umeme na vifaa vya viwandani nchini Tanzania.

Wachanganuzi wametaja hatua hiyo kuwa ya kihistoria, wakidokeza juhudi za kuongeza ushiriki katika rasilimali muhimu.

Akizungumza kuhusu makubaliano hayo, Aziz alisema mpango huo umekuwepo kwa muda mrefu na kwamba unalenga kuhakikisha Tanzania inavuna pakubwa kutokana na rasilimali yake.

Alisisitiza kuwa umiliki wa nyumbani utaimarisha uchumi wa nchi na kuchochea uwekezaji katika viwanda vinavyotumia gesi.

Wataalam wa Nishati wanaamini kuwa hatua hiyo utaimarisha ushindani na kufungua  ukurasa mpya wa maendeleo katika sekta ya gesi nchini Tanzania.

Share This Article