Kaka wawili wa kambo wako katika hatari ya kushtakiwa kwa mauaji baada ya mzee waliyeshambulia kufariki kutokana na majeraha waliyomsababishia.
Nicholas Kamau Kagecho wa umri wa miaka 54, mkazi wa Umoja, Nairobi alishambuliwa usiku wa tarehe 24 mwezi Disemba mwaka jana na kuachwa na majeraha mabaya.
Alipelekwa katika hospitali ya Metropolitan ambako alipokea matibabu ya dharura na kupatiwa rufaa hadi hospitali kuu ya Kenyatta kutokana na hali yake iliyotajwa kuwa mbaya.
Mzee huyo amekuwa akipigania maisha yake katika chumba cha wagonjwa mahututi hadi alipoaga dunia Machi 6, 2026.
Polisi walianzisha uchunguzi kuhusu shambulizi dhidi ya mzee huyo na kugundua kwamba alishambuliwa na wanawe wa kambo wawili wa kiume Brandon Githinji wa miaka 29 na Benard Lee Ngugi wa miaka 22.
Tatizo lilibainika kutokana na mzozo wa kinyumbani uliokithiri na kuishia kwenye ugomvi. Wawili hao walitiwa mbaroni Disemba 28, 2025.
Walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza siku hiyo ambapo viongozi wa mashtaka waliomba waendelee kuzuiliwa uchunguzi ukiendelea.
Kesi dhidi ya wawili hao sasa imebadilika pakubwa na maafisa husika wanasema mashtaka yamebadilika.
Brandon Githinji na Benard Lee Ngugi sasa wanakabiliwa na mashtaka ya mauaji, kinyume na sehemu nambari 203 ikisomwa pamoja na sehemu ya 204 ya kanuni za adhabu.
Uchunguzi bado unaendelea huku maafisa wa upelelezi wakikalimisha michakato muhimu ya kisheria kabla ya kuwasilisha rasmi mashtaka yaliyobadilishwa mahakamani.
Washukiwa wamezuiliwa rumande katika gereza la Industrial Area Nairobi.