Baada ya miaka mingi akiishi maisha ya starehe kupita kiasi, msanii maarufu wa Uganda Jose Chameleone ametangaza rasmi kwamba ameacha uvutaji wa sigara na unywaji wa pombe.
Akizungumza alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, jijini Nairobi, alieleza waandishi wa habari kuwa ameanza upya maisha yake.
“Mungu amenipa nafasi nyingine, kwa hiyo nimezaliwa upya,” alisema kwa sauti ya utulivu lakini yenye msisitizo. “Yote niliyokuwa nikifanya sasa yamebaki nyuma. Nimeanza maisha mapya katika awamu hii ya pili.”
Katika mahojiano ya hivi karibuni yaliyojaa hisia, Chameleone alikiri waziwazi “Nilikuwa nikibugia pombe sana, hiyo ni kweli. Nimekuwa mvutaji wa sigara maisha yangu yote. Lakini kwa ajili ya afya na maisha yangu, nimeacha. Silevi tena, sivuti tena. Nimeweka hayo pembeni kabisa.”
Msanii huyo ambaye amekuwa kwenye tasnia ya muziki kwa zaidi ya miongo miwili, alisema huu ni mwanzo mpya katika maisha yake – wakati wa “kuzaliwa upya.”
“Hii ni mara yangu ya pili kujaribu kuacha,” alisema. “Nina miaka mitatu tu kufikisha 50, kwa hiyo lazima nipunguze kasi.”
Chameleone pia alifichua sababu ya kufanya ibada ya shukrani mara aliporejea Uganda, akisema “Watu wanapaswa kujua kwamba mimi ni mtu wa Mungu. Ni Mungu aliyeniokoa hata kabla ya madaktari kufanya kazi yao.”
Kwa sasa, Chameleone yuko Nairobi kwa uchunguzi wa kiafya. Hii ni baada ya kupona kufuatia kulazwa kwa miezi kadhaa hospitalini nchini Marekani kwa matatizo ya kiafya.