Mwanamieleka maarufu John Cena alimshinda Logan Paul katika pigano lililoandaliwa Jumapili Agosti 31, 2025, ufanisi aliosherehekea kwa njia ya kipekee ya kumbusu mke wake Shay Shariatzadeh.
Cena wa umri wa miaka 48 ambaye anaendeleza ziara ya kustaafu alimshinda Paul wa umri wa miaka 30, katika pigano hilo la WWE jijini Paris nchini ufaransa.
Busu kati ya Cena na mkewe wa umri wa miaka 36 lilinakiliwa kwenye picha na video zilizosambazwa mitandaoni.
Wanamuziki Post Malone na Jelly Roll walihudhuria pigano la Cena na Paul na baada ya ushindi wakampongeza Cena.
Paul alielezea sababu ya kutaka kupigana na Cena kwenye ziara yake ya kuaga ambayo ni ari ya kuthibitisha kwamba yeye ni mwanamieleka kamili na anaweza kuiletea biashara ya mieleka mazuri.
Kwenye chapisho hilo katika mtandao wa X, Paul aliendelea kumsifia Cena akisema anapigana kwa ujuzi wa hali ya juu na kwamba hata ingawa hakuibuka mshindi, amejipatia ushindi mwingine kupitia pigano hilo.
John Cena alianzisha ziara yake ya kustaafu wakati wa uzinduzi wa kipindi cha Monday Night Raw kwenye jukwaa la mitandaoni la Netflix Januari 6, 2025.
Nyota huyo wa WWE amekuwa akipiga mieleka tangu mwaka 2018, lakini Julai 2024 alitangaza kwamba anatarajia kupigana mara 30 hadi 40 mwaka huu wa 2025 kabla ya kumaliza mwaka wake wa mwisho kama mwanamieleka.