Jeshi la Sudan limekanusha madai ya kushambulia kwa mabomu msafara wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) ukipeleka msaada katika eneo lililokumbwa na njaa katika jimbo la Darfur nchini humo.
Wapiganaji wa RSF walilaumu jeshi kwa shambulio la anga la Jumatano katika mji wa Mellit, ambao uko chini ya udhibiti wa RSF.
WFP haikutoa maelezo mengi kuhusu shambulio hilo, lakini ilisema malori matatu katika msafara huo wa magari 16 yameharibika na kushika moto.
Wafanyakazi wote waliokuwa wakisafiri katika msafara huo walikuwa salama, iliongeza.
Sudan ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwezi Aprili 2023 baada ya mzozo mkali wa madaraka kuzuka kati ya jeshi na RSF, na kusababisha moja ya mgogoro mbaya zaidi wa kibinadamu duniani.
RSF haina kikosi cha anga, lakini pande zote mbili hutumia droni.
Shambulio hilo ni la hivi karibuni zaidi katika msururu wa mashambulizi dhidi ya operesheni za kibinadamu nchini Sudan.