Mchekeshaji Jemutai amechukua hatua ambayo imeshangaza wafuasi wake mitandaoni, baada ya kufuta akaunti zake zote kwenye mitandao ya kijamii.
Haya yanajiri siku chache baada ya hafla aliyoandaa ya kuadhimisha miaka 11 ya uchekeshaji huko Eldoret ambayo inaripotiwa kutofanikiwa.
Jemutai alisema sherehe hiyo ililenga kuadhimisha miaka yake 11 ya kuchekesha Wakenya, kuiwakilisha jamii yake na kuburudisha hadhira.
Katika taarifa yake, alisema msaada aliotarajia kutoka kwa baadhi ya viongozi haukupatikana, licha ya kile alichosema kuwa ni ahadi za awali za kuhudhuria au kusaidia sherehe hiyo.
Jemutai alisema kutokuwepo kwao kulimkatisha tamaa, hasa kwa kuwa amewaona viongozi wakijitokeza kuwaunga mkono wasanii wengine.
Aliwaomba Wakenya ambao wamekuwa wakifuatilia na kuunga mkono vichekesho vyake kwa miaka 11 iliyopita wamsaidie katika kipindi hiki kigumu.
Alisema tukio hilo lilimwacha na majukumu ya kifedha ya kuwalipa watoa huduma na wabunifu walioshiriki kufanikisha sherehe hiyo.
“Bado tuna majukumu ya kutimiza kwa watoa huduma na wabunifu waliofanya kazi kwa bidii kuhakikisha sherehe hii inafanikiwa. Tafadhali simameni nami na mnisaidie kwa njia yoyote mnayoweza,” aliomba.
Mchekeshaji huyo aliwaomba watu wenye nia njema wamsaidie kwa njia yoyote wanayoweza na akatoa nambari 0708 814 820 kwa ajili ya michango.