Mwanamuziki wa Marekani Janet Jackson anaripotiwa kutoridhishwa na filamu kuhusu maisha ya marehemu kakake Michael Jackson ambaye pia alikuwa mwanamuziki.
Familia ya Jackson ilipata fursa ya kutizama filamu hiyo kwa faragha kabla ya kuzinduliwa rasmi na Janet anaripotiwa kuvutana na kakake Jermaine Jackson katika kikao hicho.
Janet anaripotiwa kukosoa mambo mengi tu kwenye filamu hiyo kama vile utaalamu wa waigizaji, mapodozi na maonyesho fulani, katika kikao hicho kilichohusisha zaidi ya watu 60 wa familia ya Jackson.
Wakati filamu hiyo ikiendelea, wengi wa watu wa familia hiyo walionekana kuifurahia huku wakicheka kuhusu matukio fulani lakini Janet kwa upande wake alikuwa akichemka.
Ilipokwisha filamu hiyo, Janet alipaaza sauti na kulalamika hadharani wakati kakake kwa jina Jermaine wa umri wa miaka 71 akasimama kumkanya.
Hatua ya Janet kulingana na wadadisi inaonyesha ugomvi wa kimya kimya ambao umekuwepo kati ya watu fulani wa jamii ya marehemu Michael Jackson.
Janet amekuwa mmoja wa wanafamilia ambao wanamuunga mkono binti ya Michael aitwaye Paris Jackson, wa umri wa miaka 27, anayekabiliana na usimamizi wa mali za babake mahakamani.
Mzozo huo umesababisha ugomvi kati ya ndugu za Jacksona, binamu zake na hata washauri ambao hawakubaliani na jinsi mali za Michael zinasimamiwa.
Filamu hiyo kuhusu maisha ya Michael Jackson iitwayo “Michael” inatizamiwa kuzinduliwa rasmi kwenye kumbi za filamu nchini Australia Aprili 23, 2026.
Mwanawe Jermaine Jackson aitwaye Jaafar Jackson, ndiye ameigiza kama marehemu Michael Jackson kwenye filamu hiyo.