Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imetakiwa kufanya kila iwezalo kuhakikisha inarejesha imani ya umma katika taasisi hiyo ambao utenda kazi wake umekuwa wa kutilia shaka siku zilizopita.
Wito huo umetolewa na Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula alipouongoza uongozi wa bunge hilo kukutana katika majengo ya bunge na Makamishna wapya wa IEBC walioapishwa Julai 11, 2025.

“Wakati wa mkutano huo, nilitoa wito kwa tume hiyo kuchukua hatua za haraka na kuanza safari ya kurejesha imani ya umma kwenye tume hiyo na kudumisha nafasi yake kama msingi wa chagzi huru, zenye usawa, zinazoweza kuthibitishwa na za kuamnika,” alisema Wetang’ula aliyeandamana na kiongozi wa wengi Kimani Ichung’wah miongoni mwa viongozi wengine wa bunge.
“Nilimkumbusha Mwenyekiti na Makamishna wa tume hiyo kuheshimu kiapo chao cha utenda kazi wakati hata nikisisitiza kuwa Wakenya wanawatarajia kutokuwa na upendeleo, kuwa waadilifu na wanataaluma katika utekelezaji wa mamlaka yao ya kikatiba.”
Ujumbe wa IEBC uliotembelea Bunge la Taifa leo Alhamisi uliongozwa na mwenyekiti wake Erastus Edung Ethekon.
