Tume Huru ya Uchaguzi na Uratibu wa Mipaka Nchini, IEBC imekanusha uwezekano wa kutathmini mipaka na kuunda maeneo mapya ya uwakilishi bungeni kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
IEBC ilibainisha hayo katika jibu ililowasilisha katika bunge la Seneti la swali lililowasilishwa na Seneta wa kaunti ya Kisii Richard Onyonka.
Onyonka aliwasilisha swali lake mbele ya bunge hilo mwezi Juni mwaka 2025 ambapo alitaka kufahamu iwapo tume hiyo ingegawa maeneo yenye wakazi wengi ili wapate uwakilishi sawa kabla ya uchaguzi mkuu ujao.
Alitaka kufahamu mipango ambayo ilikuwa imewekwa kuhusiana na ugawaji wa maeneo bunge makubwa kabla ya uchaguzi wa mwaka 2027 ili watu wapate uwakilishi sawa.
IEBC katika jibu lake ilibainisha kwamba masuala kadhaa ya kisheria ambayo hayajatatuliwa kuhusu deta na kuyoyoma kwa muda ni vikwazo vikuu vya mchakato huo.
Jibu hilo ni ishara kwamba maeneo bunge makubwa katika maeneo kama Kisii, Nyamira na Migori yatasalia yalivyo katika uchaguzi mkuu ujao.
Kaimu mkurugenzi mtendaji wa IEBC, Moses Sunkuli, alitaja uamuzi wa mahakama wa mwaka jana ambao ulipuuzilia mbali deta ya sensa ya mwaka 2019 ya maeneo bunge 14 katia kaunti za Garissa, Wajir na Mandera.
Kuhusiana na muda, katiba inaelekeza kwamba mabadiliko yoyote katika mipaka yanafaa kukamilishwa miezi 12 kabla ya uchaguzi mkuu.
Muda uliosalia kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka ujao kulingana na Sunkuli hautoshi kwani tayari tume imeanza kujiandaa kwa uchaguzi huo na haiwezi kutekeleza shughuli ya uratibu mipaka sambamba na matayarisho hayo.