Ibada ya pamoja ya wafu inaandaliwa leo Jumatatu katika Chuo Kikuu cha Masinde Muliro bewa la Webuye kuwaenzi watu 16 waliofariki katika ajali kwenye barabara ya Webuye-Kitale Machi 9 usiku.
Ajali hiyo inadaiwa kusababishwa na dereva wa lori la masafa marefu ambaye alipoteza mwelekeo na kugonga magari kadhaa pamoja na wapita njia.
Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula na viongozi mbalimbali hasa kutoka eneo la Magharibi ni miongoni mwa waliotarajiwa kuhudhuria ibada hiyo.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Wetang’ula aliongoza hafla ya kuchangisha fedha za kuwasaidia waathiriwa katika shule ya sekondari ya Sipala ambapo Rais William Ruto alitoa mchango wake wa shilingi milioni 7.5.
Wetang’ula alitoa mchango wa shilingi milioni moja huku wabunge na viongozi wengine waliokuwepo pia wakitoa michango.
Kiongozi huyo alihakikishia familia za waathiriwa kwamba wataendelea kusimama nao hadi kila familia itakapozika mpendwa wao.
Watu wengine kadhaa walijeruhiwa kwenye ajali hiyo na wanaendelea kupokea matibabu.
Madereva wametakiwa kuwa waangalifu ili kuepuka kusababisha maafa ambayo yamekuwa donda sugu kwenye barabara za humu nchini kwa muda mrefu.