Gavana Sakaja akosoa agizo la Seneti la kutaka akamatwe

Seneti iliagiza Gavana huyo akamatwe na kuwasilishwa mbele ya kamati ya bunge hilo kwa madai ya kukaidi maagizo kadhaa ya kufika mbele yake.

Tom Mathinji
2 Min Read
Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja.

Gavana wa Nairobi  Johnson Sakaja amepuuzilia mbali agizo lililotolewa na Bunge la Seneti kwa Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja la kutaka akamatwe.

Seneti iliagiza Gavana huyo akamatwe na kuwasilishwa mbele ya kamati ya bunge hilo kwa madai ya kukaidi maagizo kadhaa ya kufika mbele ya kamati hiyo.

Hata hivyo, kupitia kwa taarifa siku ya Jumatatu, Sakaja alidai kuwa hatua ya kutofika mbele ya kamati ya Bunge la Seneti ilitokana na mwongozo wa Baraza la Magavana, lililowashauri Magavana kutofika mbele ya kamati fulani hadi masuala yaliyoibuliwa na baraza hilo yatakapotatuliwa.

“Swala lililopo sio la kibinafsi kuhusu Gavana Sakaja, lakini ni swala linaloshughulikiwa kwa pamoja na Baraza la Magavana,” alisema Sakaja kwenye taarifa hiyo.

Aliongeza kuwa mzozo kati ya Magavana na Maseneta unapaswa kusuluhishwa kitaasisi na wala sio kwa kumlenga Gavana binafsi.

Wakati huo huo, Sakaja ambaye pia ni Seneta wa zamani wa Nairobi alidokeza kuwa awali alifika katika kamati kadhaa za Seneti ikiwa ni pamoja na ile kuhusu Ardhi na Mazingira juma lililopita.

Alishutumu jinsi maafisa wa polisi walivyotumwa kumkamata, akihoji uhalali wa operesheni hiyo.

“Hakuna haja ya kuzua kizaazaa wakati wa usiku.”

Mnamo siku ya Jumatatu usiku, maafisa wa polisi walizingira afisi za serikali ya kaunti ya Nairobi zilizoko katikati mwa jiji la Nairobi wakitaka  kumkamata Sakaja.

Hatua hiyo ilifuatia agizo la Seneti lililomwagiza Inspekta Mkuu wa Polisi kumwasilisha Gavana huyo mbele ya kamati ya Seneti.

Sakaja anahitajika kujibu maswali ya ukaguzi wa matumizi ya fedha ya kaunti hiyo mwaka 2024/25.

Share This Article