Tume ya Filamu Nchini, KFC kwa ushirikiano na waandaaji wa tuzo za kimataifa za filamu na vipindi vya runinga za Kalasha wanaonyesha filamu ambazo zimeteuliwa kuwania tuzo katika awamu ya 14 ya tamasha hizo.
Maonyesho hayo yalianza wikendi ambayo imekwisha ambapo Ijumaa waliofika katika ukumbi wa maonyesho ya filamu wa Anga walitizama Boda Love na She gets me. Filamu zilizoonyeshwa Jumamosi ni 2 Asunder na Safari.
Jumapili KFC ilionyesha filamu tatu ambazo ni Cards on the table, Sarah na Memory of Princess Mumbi huku maonyesho ya kazi nyingine zilizoteuliwa kuwania tuzo yakiendelea wiki nzima hadi Ijumaa Aprili 17, 2026.
Filamu zitakazoonyeshwa wiki hii katika ukumbu wa Anga ni pamoja na Own Goal, Deafinately Heard, Spin to Loose, Safari, The Inkidongi, Lore, S.He Gets Me, The Big Sad Nairobi, Kito and Chacha: The Leader, Cards on the Table, Boda Love, Family Vacation na Makosa ni yangu.
Tamasha la mwaka huu la Kalasha ambalo hujumuisha soko, maonyesho na tuzo litaandaliwa Aprili 28 hadi Mei 2, 2026 katika jumba la KICC jijini Nairobi.
Tuzo za mwaka huu zitahusisha pia wanaojihusisha na kubuni maudhui mitandaoni kupitia vitengo viwili, kimoja cha maudhui yaliyokuwa na athari chanya na kingine kikiwa muunda maudhui kidijitali bora zaidi.
Maudhui ya mwaka huu ni “Kubuni Tamaduni: Kubuni upya usimulizi, fremu moja baada ya nyingine.”