Familia zatamaushwa na ukimya wa wapendwa wao nchini Urusi

Ukosefu wa mawasiliano ya wazi umeziacha familia hizi gizani, na sasa zinaiomba serikali kuingilia kati

Marion Bosire
3 Min Read

Familia kadhaa katika Bonde la Ufa nchini Kenya zina hofu na huzuni kufuatia ripoti kwamba wapendwa wao waliokwenda Urusi wamepotea, huku wengine wakihofiwa kufariki katika vita vinavyoendelea kati ya Urusi na Ukraine.

Ukosefu wa mawasiliano ya wazi umeziacha familia hizi gizani, na sasa zinaiomba serikali kuingilia kati haraka.

Katika vijiji mbalimbali vya Uasin Gishu na maeneo ya jirani, hofu na sintofahamu vimetanda. Familia zinasema vijana wao waliondoka nchini wakitafuta fursa bora za ajira, lakini wakatoweka katika nchi ya kigeni, Urusi.

Miongoni mwao ni Josephine Chepngetich, ambaye mwanawe Keith Kiplagat aliondoka nchini Oktoba mwaka jana akitarajia kupata ajira nje ya nchi.

Chepngetich anasema mawasiliano na mwanawe yalikatika ghafla tarehe 28 Novemba, baada ya kumwambia kuwa amehamishiwa katika kambi nyingine.

Sasa anahofia kwamba huenda mwanawe hayuko hai tena. Anadai kuwa safari ya mwanawe iliandaliwa na mtu anayejulikana kama Collins, ambaye inadaiwa aliwashawishi kwa ahadi za kazi nje ya nchi.

Badala yake, familia nyingi sasa zinaamini kuwa vijana hao waliingizwa katika vita vya Ukraine.

Mbali na maumivu ya kihisia, familia hizi pia zinakabiliwa na mzigo mkubwa wa kifedha.

Chepngetich anasema alitumia akiba yake yote ya pesa aliyokuwa ameweka kando kwa ajili ya kujenga nyumba kugharamia safari ya mwanawe.

Wanaharakati wa haki za binadamu sasa wanasihi serikali kuchukua hatua za haraka. Mustapha David Simiyu anasisitiza haja ya kuwepo kwa mfumo rasmi wa kusaidia familia kupata taarifa sahihi.

Mwezi Februari mwaka huu, familia zilizoathirika zilifanya maandamano nje ya Bunge jijini Nairobi, zikidai majibu na kurejeshwa kwa wapendwa wao.

Serikali ya Kenya tangu wakati huo imeanzisha mazungumzo na Urusi kuhusu suala hilo. Kufuatia ziara ya kidiplomasia nchini Urusi, Waziri Mkuu Msaidizi Musalia Mudavadi alisema kuwa raia wa Kenya hawataruhusiwa tena kujiunga na jeshi la Urusi.

Hata hivyo, hatima ya wale ambao tayari wako katika mzozo huo bado haijulikani.

Ripoti zinaonyesha kuwa Wakenya zaidi ya 1,000 huenda walipelekwa vitani, wengi wao wakidaiwa kupotoshwa kwa ahadi za kazi zenye malipo mazuri. Familia zilizotafuta msaada kutoka Ubalozi wa Urusi jijini Nairobi zinasema hazijapata majibu ya kuridhisha.

Viongozi wa jamii sasa wanatoa wito kwa Rais William Ruto kuingilia kati na kuanzisha mfumo rasmi wa kusaidia familia kufuatilia ndugu zao waliopotea.

Share This Article