DPP aapa kukabiliana vikali na jinamizi la ufisadi nchini

Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma inasema inasalia imara kuhakikisha visa vyote vya ufisadi na uhalifu wa kifedha vinashughulikiwa haraka.

Martin Mwanje
1 Min Read
Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Renson Ingonga (kushoto)

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga amesisitiza dhamira ya ofisi yake kupambana vikali na jinamizi la ufisadi na uhalifu wa kifedha nchini.

Ingonga ameyasema hayo wakati wa mkutano wa kuangazia mageuzi ya uongozi uliowaleta pamoja maafisa wa idara mbalimbali serikalini na wale wa Shirika la Fedha Duniani, IMF. 

Mkutano huo uliongozwa na Katibu katika Wizara ya Fedha Dkt. Chris Kiptoo.

Kulingana na Ingonga, ofisi yake imeendelea kutekeleza hatua madhubuti zinazokusudia kuhakikisha wahusika wa makosa yanayohusiana na ufisadi ikiwa ni pamoja na visa vya utakatishaji wa fedha wanakabiliwa ipasavyo na mkono wa sheria.

“Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) inasalia imara kuhakikisha visa vyote vya ufisadi na uhalifu wa kifedha vinavyokidhi kiwango cha ushahidi vinashughulikiwa haraka na mashtaka kufunguliwa,” aliahidi Ingonga wakati wa mkutano huo.

Alitoa mfano wa kitengo cha kupambana na utakatishaji wa fedha na kutwaa mali kilichoanzishwa katika ofisi yake kuwa mfano wa mageuzi yanayolenga kukabiliana na ufisadi na uhalifu wa kifedha nchini.

 

Share This Article