Chama cha upinzani nchini Tanzania Chama cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA kimetishia kurai wafuasi wake kote nchini humo kutekeleza maandamano iwapo mwenyekiti wa chama hicho Tundu Lissu hatoachiliwa.
Hayo yalibainika leo kwenye mjadala ulioandaliwa mtandaoni wakati Tundu Lissu, aliyekamatwa na kuzuiliwa kwa madai ya uhaini, anatimiza mwaka mmoja kizuizini.
Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara, John Heche, aliitisha kampeni maalum kuanzia leo inayolenga kuzishinikiza mamlaka kumwachilia huru Lissu.
Heche alifafanua kwamba iwapo serikali haitatekeleza matakwa yao baada ya kampeni hiyo, basi chama cha CHADEMA kitaitisha maandamano kote nchini Tanzania.
“Hatua ya pili tutakayoenda, kama hawatotusikiliza hatuoendelea kukaa kimya na kunyamaza na kulia, tutaitisha maandamano makubwa nchi nzima wasikie na wamuachie Tundu Lissu,” alisema Heche aliyeonekana mwenye hasira.
Lissu alikamatwa tarehe kama ya leo Aprili 9, 2025 na maafisa wa polisi katika wilaya ya Mbinga, mkoa wa Ruvuma alipokuwa akiendeleza kampeni yake ya “No Reforms No Election”.
Baadaye alisafirishwa hadi Dar es salaam ambapo alifunguliwa kesi ya uhaini na uchochezi.