Wadau katika sekta ya Kilimo wamekubaliana kuharakisha miswada muhimu ya Kilimo na mageuzi yanayolenga kupunguza uagizaji bidhaa kutoka nje, kuimarisha uzalishaji nchini na kutafuta masoko ya kimataifa.
Akizungumza baada ya kushiriki mkutano wa ngazi za juu ulioleta pamoja Taasisi za Serikali (SAGAs) na kamati za Bunge la Taifa na lile la Seneti kuwianisha Sheria, sera na vipaumbele kwenye bajeti kuhakikisha utoshelevu wa chakula na ukuaji wa mauzo ya nje, Waziri wa Kilimo Mutahi Kagwe, alisisitiza kuwa hatua za kisheria ni nguzo kuu katika uzalishaji, uuzaji nje ya nchi, akionya kuwa Kenya Iko katika hatari ya kupoteza ajira na fursa za somo iwapo uongezaji dhamani hautatekelezwa.
“Kuna mwingilio wa kisheria ambao ni muhimu katika kuongeza uuzaji nje wa bidhaa na kupunguza uagizaji bidhaa kutoka nje. Ili kufanikiwa katika masoko kama vile China, lazima tuongeze thamani kwenye bidhaa hapa nyumbani,” alisema Kagwe.
Kwa upande wake katibu wa Ustawi wa Mifugo Jonathan Mueke, alielezea umuhimu wa kuwianisha bunge na ajenda ya mageuzi ya Wizara hiyo akidokeza kuwa Sheria zilizopigwa na wakati, zinaendelea kudumaza ukuaji wa sekta hiyo.
“Sheria zetu lazima ziwe za kisasa na zinapaswa kubuni mazingira yanayokua. Lazima tushirikiane na bunge kuharakisha miswada muhimu,” alisema Mueke.
Mkutano huo ulikubaliana kutambua sheria zilizo mbele ya Bunge ili kuharakisha mageuzi katika mifumo ya deta ya mimea, mifugo na utoshelevu wa chakula na kuiweka Kilimo kuwa kichocheo Kikuu Cha uchumi wa kenya.