Mashindano ya kuwania Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kwa chipukizi chini ya umri wa miaka 17 yanayoendelea nchini Morocco, ni dhihirisho la hatua mwafaka zilizochukuliwa na Serikali ya Kifalme nchini Morocco katika ukuzaji vipaji.
Taifa hilo la Kaskazini mwa Afrika, kupitia kwa Ajenda ya mwaka 2009 ya Mfalme Mohammed wa sita wa Morocco, linakusudia kuwa kielelezo barani Afrika.
Hiyo ni kupitia ujumuishwaji wa wachezaji wanne wanaotokea katika Akademia ya Mohammed 6, soka ya chipukizi ikiwa mojawapo wa ruwaza ya muda mrefu ya makuzi ya vipaji vya soka.
Akademia ya Mohammed 6 ilizinduliwa mwaka 2009 ili kuleta utaalam na ufundi wa soka kupitia kuwepo kwa miundombinu ya kisasa.

Leo hii ukitembea Morocco kufuatilia AFCON kwa chipukizi ya umri wa miaka 17, utapata wachezaji wapya kama vile Ibn Salah Oualid, Boughazir Adam, Harouch Mohamed na Ezzarky Ayman, wakiwa baadhi ya wachezaji waliotokea katika mifumo ya chipukizi.
Wanandinga hao wanafuata nyayo za wachezaji nyota katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 2022, kama vile Youssef En-Nesyri, Nayef Aguerd, na Azzedine Ounahi.