Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa awasili Kenya kwa ziara rasmi ya siku mbili, huku ziara hiyo ikitarajiwa kupanua ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.
Akimpokea Rais huyo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, alisema ziara hiyo inathibitisha uhusiano wa muda mrefu na kujitolea kwa mataifa hayo mawili katika ustawi wa kiuchumi, utangamano wa kikanda na maendeleo ya pamoja.
Mkutano baina ya Rais Mnangagwa na mweyeji wake Rais William Ruto, unalenga kubuni fursa mpya za kibiashara na uwekezaji, pia ukiimarisha ushirikiano katika sekta muhimu ikiwa ni pamoja na kilimo, afya, elimu, uchukuzi na ulinzi.
Kupitia ukurasa wake wa X, Rais Mnangagwa alisema anatazamia mazungumzo yatakayozaa matunda na kuwafaidi raia wa Zimbabwe na Kenya.