Bodi ya Hakimiliki Kenya, KECOBO imewaalika wananchi na wadau kuwasilisha maoni kuhusu ufaafu wa waombaji sita wa leseni za kufanya kazi kama Mashirika ya Usimamizi wa Haki za Pamoja, CMOs.
Bodi hiyo imesema maoni ya maandishi na mawasilisho ya ana kwa ana yatasaidia kutathmini waombaji hao kwa mujibu wa Kanuni za Hakimiliki (Usimamizi wa Haki za Pamoja) za mwaka 2020.
Waombaji hao ni Music Copyright Society of Kenya (MCSK) Ltd, Film Makers Rights Achievers of Kenya (FRAK) Ltd, KAMP Copyright and Related Rights Limited, Boralways Limited, Performing and Audio-visual Rights Society of Kenya (PAVRISK) Ltd na Collective Management Services Ltd.
Maombi yao yanahusu usimamizi wa haki katika nyanja mbali mbali, kama kazi za muziki, utayarishaji wa kazi za sauti na picha, rekodi za sauti, wasanii wa utendaji, waandishi, watunzi, wachapishaji, watayarishaji na filamu.
KECOBO itafanya kikao cha umma Jumatano, Desemba 2, 2026, kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 7 mchana katika ukumbi wa SHA.
Wadau wanaweza kuwasilisha maoni yao kwa barua pepe kupitia cmos@copyright.go.ke.
Maoni ya maandishi yanapaswa kuwasilishwa kabla ya saa 11 jioni siku hiyo hiyo. Nakala za maandishi pia zinaweza kuwasilishwa katika mapokezi ya KECOBO, orofa ya tano ya jengo la SHA, barabara ya Ragati/Ngong, Nairobi.
KECOBO ina jukumu la kutoa leseni na kusimamia Mashirika ya Usimamizi wa Haki za Pamoja nchini Kenya.