Safari ya Kenya katika mashindano ya ulimbwende ya Miss Universe 2026 imefikia tamati bila kupata taji hilo, huku mwakilishi wa Puerto Rico, Jennifer Barreto, akishinda kwenye fainali iliyofanyika mjini San Juan, nchini Puerto Rico.
Shirika la Miss Universe Kenya limewashukuru Wakenya kwa kumuunga mkono mwakilishi wao, Jean Ojiro, katika kipindi chote cha mashindano hayo, ambayo Kenya ilirejelea baada ya kukosa mwaka jana.
Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii, shirika hilo lilipongeza Wakenya kwa kupiga kura, kuhamasisha wengine kushiriki na kuunga mkono kampeni ya Ojiro kimataifa.
Lilisema timu hiyo ilijitahidi licha ya kutoafikia matokeo iliyokuwa ikiyatarajia, huku likieleza kujivunia jinsi Kenya iliwakilishwa katika jukwaa la kimataifa.
Pia lilimpongeza Ojiro kwa kuiwakilisha Kenya kwa heshima, ujasiri na kujitolea, likisema mashindano hayo yalitoa fursa ya kuonyesha utamaduni, ubunifu na simulizi za nchi.
Wakati huo huo, Barreto wa umri wa miaka 27 alishinda taji hilo baada ya kuwazidi washiriki 115.
Mwanasaikolojia na mwanamitindo huyo aliweka historia kwa kuwa mwanamke wa kwanza aliyeolewa na mwenye mtoto kuwahi kushinda taji hilo tangu mashindano hayo yalipofunguliwa kwa wanawake walioolewa na kina mama mwaka 2023.
Pia amekuwa mwanamke wa sita kutoka Puerto Rico kushinda taji la Miss Universe, akimrithi Fatima Bosch wa Mexico.