Nyota wawili wa kike wa muziki nchini Tanzania Nandy na Zuchu wanaonekana kuwa katika kile ambacho kinaweza kurejelewa kama mvutano au ushindani mkali.
Haya yanatokana na tarehe ambayo Nandy amepanga kutoa kazi yake mpya, albamu kwa jina 911, ambapo baada yake kutangaza ujio huo, Zuchu na mumewe Diamond Platnumz nao wamepanga kuandaa tamasha ya kusherehekea siku ya kuzaliwa ya Zuchu siku hiyo hiyo.
Mashabiki na watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini Tanzania wanawanyoshea Zuchu na Diamond kidole cha lawama kwa kile wanachokitaja kuwa jaribio la kuhujumu utoaji wa albamu ya Nandy.
Wakosoaji wanasema kwamba Diamond pia alitangaza na kusifia hadharani kazi mpya za wasanii Zuchu, Jux na Alikiba zinazotarajiwa kutoka siku hiyo hiyo ambayo ni Novemba 27, 2026.
Hata hivyo Zuchu amekanusha madai ya hujuma ya kimakusudi akisisitiza kwamba yeye na mume wake Diamond Platnumz hawakufahamu kuhusu mipango ya Nandy awali.
Zuchu amechagua kuahirisha sherehe yake ya siku ya kuzaliwa labda kama njia ya kupoza moto uliokuwa ukitishia kuwaka katika tasnia ya burudani nchini humo.
Mgongano huu wa hivi punde kati ya wasanii hao unajiri siku chache tu baada ya Nandy kuzua mjadala alipodhihirisha kutofurahishwa na ulinganishi kati yake na Zuchu unaotekelezwa na watu fulani na akaishia kujipiga kifua kwamba yeye ndiye mwanamuziki bora wa kike Tanzania.