KAMP yaahirisha mirabaha kisa ukosefu wa fedha

Shirika hilo limewaomba wanachama radhi kwa usumbufu uliosababishwa na kuahirishwa kwa malipo hayo.

Marion Bosire
1 Min Read
Japheth Kasanga, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, KAMP

Shirika la Usimamizi wa Pamoja wa Hakimiliki kwa Watayarishaji Muziki Nchini Kenya, KAMP, limeahirisha malipo ya mirabaha kwa wanachama wake kutokana na ukosefu wa fedha za kutosha kugharamia zoezi hilo.

Katika taarifa ya Novemba 16, 2026, KAMP ilisema usambazaji wa mirabaha uliokuwa umepangwa kufanyika Oktoba 31 hautaendelea kama ilivyotarajiwa.

Shirika hilo lilieleza kuwa bodi mpya iliyoundwa inashughulikia masuala ambayo yameathiri upatikanaji na utoaji wa fedha hizo, ili kuhakikisha malipo yanafanyika haraka iwezekanavyo.

KAMP pia ilitambua matarajio ya wanamuziki na wanachama wengine wanaostahili kulipwa ambao waliwasilisha na kusasisha kazi zao za muziki kwa ajili ya zoezi hilo.

Shirika hilo liliwaomba wanachama radhi kwa usumbufu uliosababishwa na kuahirishwa kwa malipo hayo, likihakikishia kuwa mirabaha inayostahili kulipwa itahesabiwa ipasavyo na kugawiwa kwa wanufaika wanaostahili.

Aidha, KAMP ilisema itatangaza ratiba mpya ya malipo mara tu mipango muhimu itakapokamilika.

Hata hivyo, shirika hilo halikutaja tarehe maalumu ya kuanza tena kwa usambazaji wa mirabaha.

Share This Article