Rais William Ruto amesema utawala wake unato kipaumbele kwa miradi muhimu ya miundombinu katika kaunti ya kiambu.
Kiongozi wa taifa alisema, ujenzi wa barabara ya Kiambu kuwa yenye safu mbili pamoja na ujenzi wa barabara ya moja kwa moja ya Nairobi – Thika, utapunguza msongamano wa uchukuzi na kuboresha uunganishaji wa Jiji la Nairobi na maeneo mengine.
Rais Ruto aliyasema hayo Ijumaa aliposhiriki mazungumzo na viongozi wa kaunti ya Kiambu, ambapo walijadili utekelezaji wa miradi kadhaa ya maendeleo ili kuchochea ukuaji na kuimarisha utoaji wa huduma.
“Tutahakikisha kila eneo la Kenya linanufaika kwa usawa kutokana na ajenda yetu ya mabadiliko. Hakuna kaunti, jamii ama eneo litaachwa nyuma,” alisema Rais Ruto.
Mbunge wa Kikuyu aliyepia kiongozi wa wengi katika Bunge la Taifa Kimani Ichung’wa, aliwaongoza viongozi hao kwenye mkutano huo ambao umejiri huku joto la kisiasa hapa nchini likipanda, kabla ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2027.