Kiongozi wa chama cha Linda Mwananchi Edwin Sifuna anatarajiwa kuzuru nchini Marekani kutafuta uungwaji mkono wa wapiga kura wa ughaibuni pamoja na kuchangisha hela za kampeni.
Sifuna na msafara wake wanatarajiwa kuzuru majimbo kadhaa nchini Marekani kuanzia Novemba 20, kukutana na Wakenya wanaoishi nchini humo.
Seneta huyo wa Nairobi anapigiwa upato kuwa mpeperushaji wa bendera ya upinzani kukabiliana na Rais William Ruto katika uchaguzi wa urais mwakani.
Yeye ni mmoja wa viongozi wa upinzani wanaotazamia kumbandua Rais Ruto madarakani mwakani.
Wengine ni Kalonzo Musyoka wa chama cha Wiper, Dkt. Fred Matiang’i wa chama cha Jubilee na kiongozi wa chama cha DCP Rigathi Gachagua.
Siku chache zilizopita, Sifuna alikutana na Gachagua nyumbani kwake Wamunyoro, ila maelezo ya kina kuhusu walichokijadili wakati wa mkutano huo hayajabainika.
Ilivyo kwa sasa, haijulikani ni nani kati ya viongozi hao wa upinzani atakayegombea urais wakati kila mmoja akivutia kamba upande wake.
Rais Ruto ameupuzilia mbali upinzani akisema hauna ajenda yoyote ya kuwanufaisha raia isipokuwa kutimiza maslahi yao ya binafsi.
Ameongeza yuko tayari kukabiliana na yeyote atakayeteuliwa na upinzani kumenyana naye katika uchaguzi mkuu ujao akisema atambwaga asubuhi na mapema.