Davido na Chioma wawasili Tanzania, wapokelewa na Diamond na Zuchu

Anaaminika kuwa nchini humo kwa ajili ya kumalizia video ya wimbo wao mpya wa pamoja.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanamuziki nyota wa mtindo wa Afrobeats kutoka Nigeria, Davido na mkewe Chioma, waliwasili kwa kishindo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Wawili hao walipokelewa kwa njia kubwa iliyoandaliwa na mwanamuziki nyota wa Bongo Flava, Diamond Platnumz, pamoja na mpenzi wake Zuchu.

Katika ishara ya urafiki na mshikamano, Diamond alifika mwenyewe kumpokea Davido na kumwandalia msafara wa magari ya kifahari, likiwemo gari lake maarufu aina ya Rolls-Royce Cullinan lenye rangi ya bluu.

Mapokezi hayo ya kifahari yameibua furaha kubwa miongoni mwa mashabiki, huku wengi wakikumbuka ushirikiano wao mkubwa wa mwaka 2014 kupitia wimbo maarufu Number One.

Ukaribu ulioonekana kati ya nyota hao wawili wa muziki barani Afrika umeibua hisia na mijadala kwenye mitandao ya kijamii kuhusu uwezekano wa kuimba wimbo mwingine kwa pamoja.

Hata hivyo, ratiba kamili ya ziara ya Davido nchini Tanzania bado haijawekwa wazi, lakini anaaminika kuwa nchini humo kwa ajili ya kumalizia video ya wimbo wao mpya wa pamoja.

Mwanamitandao wa Tanzania Mwijaku alifichua katika siku chache zilizopita kwamba kulikuwa na kazi ya ushirikiano kati ya Davido na Diamond iliyokuwa ikiendelea kuandaliwa.

Share This Article