Nadhari ya wengi katika kanda ya Afrika Mashariki leo Ijumaa imeelekezwa katika jiji la Mwanza katika nchi jirani ya Tanzania.
Kisa na maana? Mwanawe Rais William Ruto, Charlene Ruto na mpenziwe Isaya Yunge wamepangiwa kufunga ndoa katika hafla inayotarajiwa kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali mashuhuri.
Rais Ruto tayari ametua jijini Mwanza kushuhudia kwa mboni za macho yake, mwanawe akiasi useja.
Mkewe, Rachel Ruto, alikuwa mwenye shughuli nyingi jana Alhamisi, akichangia maandalizi ya mwisho ya mwanawe kuingia katika ndoa takatifu.
Harusi ya Charlene na Isaya imepangwa kufanyika katika ufukwe wa hoteli ya Malaika Beach Resort jijini Mwanza.
Charlene aliwasili jijini humo juzi Jumatano akitumia ndege ya kibinafsi kabla ya kusafirishwa na msafara wa magari ya kifahari hadi hotelini.
Novemba 3, 2026, binti huyo aliandaliwa hafla ya kumfunza mawili matatu kabla ya kufunga ndoa ambapo wahudhuriaji walivaa mavazi ya rangi nyeupe na kahawia.
Awali, Charlene na Isaya walifanya sherehe ya mahari na kuvishana pete za uchumba Agosti 8, 2026 nyumbani kwa Rais Ruto huko Kilgoris, kaunti ya Narok nchini Kenya.
Sherehe hiyo ya uchumba iliwakutanisha ndugu na jamaa wa pande zote mbili, ikiwa ni sehemu ya taratibu za kimila kabla ya wawili hao kuingia rasmi kwenye ndoa.
Sasa wengi wanaangazia jiji la Mwanza, ambako familia hizo mbili kwa mara nyingine zitaungana katika harusi ya wanao.
Tunawatakia wawili hao kila la heri wanapoanza maisha pamoja kama wanandoa.
Taarifa hii imechangiwa na Marion Bosire