Iran imesema matokeo ya uchaguzi wa katikati ya muhula nchini Marekani yanaashiria kuwa Wamarekani hawaungi mkono uamuzi wa Rais Donald Trump kuanzisha vita dhidi ya nchi hiyo.
Kauli hiyo imetolewa na Mohammad Bagher Ghalibaf, ambaye ni mkuu wa timu ya Iran katika mazungumzo na Marekani. Amesema matokeo ya uchaguzi huo yanapaswa kuwa ujumbe kwa utawala wa Trump kwamba wananchi hawataki kuendelea na vita.
Ghalibaf amemuonya Trump kuwa kupuuza ujumbe huo wa wapiga kura kunaweza kuisababishia Marekani hali mbaya zaidi, akitumia kauli ya “jinamizi”.
Kwa upande wake, Trump amekiri kuwa vita dhidi ya Iran vilichangia kwa kiasi fulani kushindwa kwa chama chake cha Republican katika uchaguzi huo, uliofanyika Jumanne.
Hata hivyo, katika mahojiano na gazeti la The Wall Street Journal, Trump amesema hajutii uamuzi wa kuanzisha vita hivyo na kwamba angechukua hatua hiyo tena kama angepewa nafasi nyingine.
Wakati huohuo, juhudi za kidiplomasia za kufikia makubaliano ya kusitisha vita zinaendelea, lakini hali ya usalama katika eneo la Ghuba bado ni tete. Meli kadhaa zimeripotiwa kushambuliwa katika Mlango-Bahari wa Hormuz, mojawapo ya njia muhimu zaidi za usafirishaji wa mafuta duniani.
Taarifa ya BBC