Geoffrey Chagga ambaye alikuwa meneja wa wasanii wawili wa kundi la Radio & Weasel nchini Uganda, amedai kuwa marehemu mwanamuziki Mowzey Radio alikuwa raia wa Burundi.
Chagga anasema alikuwa na ufahamu wa karibu wa historia ya familia ya mwanamuziki huyo na mizozo ya kimila iliyojitokeza baada ya kifo chake.
Akizungumza kwenye mahojiano, meneja huyo wa zamani alisema kwamba alimsaidia sana Mowzey na kumtambulisha katika tasnia ya burudani nchini humo.
Chaga aliongeza pia kwamba dadake Radio wa asili ya Burundi alihusika katika mvutano kuhusu namna mwili wa mwanamuziki huyo ulipaswa kushughulikiwa kwa kuzingatia mila zao.
Hata hivyo, Chagga hakutoa maelezo zaidi ya kuthibitisha zaidi madai yake kuhusu uraia wa mwanamuziki huyo, huku mwili wake ukizikwa nyumbani kwawazazi wa mamake huko Kagga, Nakawuka Wilaya ya Wakiso.
Mowzey Radio, ambaye jina lake halisi lilikuwa Moses Nakintije Ssekibogo, alikuwa mmoja wa wanamuziki wawili waliounda kundi maarufu la muziki nchini Uganda la Uganda la Radio & Weasel. Wa pili ni kaka mdogo wa Jose Chameleone Douglas Mayanja au Weasel Manizo.
Radio alifariki Februari 1, 2018, baada ya kupata majeraha ya kichwa katika ugomvi uliotokea kwenye baa moja mjini Entebbe.