Oburu asherehekea siku ya kuzaliwa akiwa hospitalini

Siku ya kuzaliwa kwa Oburu inasadifiana na siku ambayo aliyekuwa kiongozi wa ODM Raila Odinga alifariki akipokea matibabu nchini India.

Tom Mathinji
1 Min Read
Oburu asherehekea siku ya kuzaliwa akiwa hospitalini.

Kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) Oburu Oginga, leo Alhamisi amesherehekea siku ya kuzaliwa akiwa katika Nairobi Hospital, ambako anaendelea kupokea matibabu.

Oburu ambaye amefikisha umri wa miaka 83, alisema ana matumaini kwamba atapata nafuu na kuondoka hospitalini, akidokeza kuwa madaktari wake wamemshauri achukue mapumziko hadi afya iimarike.

Siku ya kuzaliwa kwa Oburu inasadifiana na siku ambayo aliyekuwa kiongozi wa ODM Raila Odinga alifariki akipokea matibabu nchini India.

Huku akisherehekea siku hiyo muhimu kwake, hafla ya kuadhimisha mwaka wa kwanza tangu kufariki kwa Raila ilikuwa ikiendelea katika Kang’o ka Jaramogi kaunti ya Kisumu.

Oburu alitaja siku hiyo kuwa iliyo na mchanganyiko wa furaha na huzuni, furaha ya kuzaliwa kwake na huzuni ya kumpoteza ndugu yake Raila Odinga.

Kiongozi huyo wa ODM alishukuru familia yake, wahudumu wa Nairobi Hospital, wanachama wa ODM na wafanyakazi wake wa kibinafsi kwa kuandaa sherehe hiyo pamoja na kumsaidia anapoendelea na matibabu.

Share This Article