Chameleone atangaza rasmi tamasha yake

Alijibu wakosoaji na kueleza maono yake kuhusu tamasha hiyo kubwa ijayo.

Marion Bosire
1 Min Read

Gwiji wa muziki nchini Uganda, Jose Chameleone, aliwasili kwa kishindo katika uwanja wa Lugogo Cricket Oval jana kwa kutumia helikopta, kutangaza rasmi tamasha yake inayotarajiwa kufanyika Desemba 4, 2026.

Msanii huyo mashuhuri alishuka kutoka kwenye helikopta akiwa amevalia mavazi ya kitamaduni ya kifahari na taji la dhahabu, kisha akahutubia kundi kubwa la wanahabari na mashabiki katika uwanja huo utakaoandaa tamasha hiyo.

Alijibu wakosoaji na kueleza maono yake kuhusu tamasha hiyo kubwa ijayo.

Mkutano huo na wanahabari ulidhihirisha umoja, huku Chameleone akiwa ameandamana na familia yake pamoja na watu mashuhuri katika tasnia ya muziki. Ndugu zake Weasel na Pallaso na mama yao, walikuwa kando yake.

Chameleone alitumia fursa hiyo kumpongeza Weasel hadharani kwa kusitisha shughuli zake binafsi ili kumhudumia alipokumbwa na dharura ya kiafya hivi karibuni.

Wanamuziki wengine wakubwa kama Bebe Cool na Spice Diana, pia walihudhuria mkutano huo, Bebe Cool akiwataka wananchi kumwonyesha Chameleone huruma na mshikamano.

Mbali na matangazo kuhusu muziki, Chameleone alizungumzia hali yake ya kiafya, akifichua kuwa anapanga kurejea Marekani kwa matibabu maalumu ya tatizo linaloathiri kongosho lake mara tu baada ya tamasha hilo.

Wawakilishi wa kampuni za Bar Aviation na Rose Foam Mattresses walithibitisha kuwa kampuni hizo zitafadhili pakubwa tukio hilo la kihistoria.

Share This Article