Naibu Mkuu wa Polisi wa Afrika Kusini amejiuzulu huku akikabiliwa na madai ya kushiriki ufisadi na ubakaji, ambayo ameyakanusha.
Shadrack Sibiya, alitarajiwa kuchukuliwa hatua za kinidhamu siku ya Jumatatu, lakini mawakili wake waliwasilisha kujiuzulu kwake kabla ya kuanza kwa mchakato huo.
Kwa sasa Sibiya anazuiliwa gerezani akikabiliwa na kosa la ubakaji. Kusikilizwa kwa maombi yake ya kutaka kuachiliwa kwa dhamana kumeahirishwa hadi Oktoba 13,2026.
Afisa huyo wa polisi amekuwa sehemu ya uchunguzi wa Tume ya Idara ya Mahakama kuhusu ufisadi ndani ya idara ya polisi ya Afrika Kusini na ushirikiano wao na magenge ya wahalifu.
Katika tume hiyo, Sibiya ameshtumiwa kupokea kiwango kikubwa cha fedha na zawadi kutoka kwa wahalifu, madai ambayo yeye mwenyewe ameyakanusha.