Almorie Sophia Nagayi, mrembo mwenye umri wa miaka 19, ndiye mshindi wa taji la Miss Uganda msimu wamwaka 2026/27, kufuatia hafla ya fainali iliyofanyika Jumamosi, Oktoba 10, 2026, katika Hoteli ya Sheraton, jijini Kampala.
Nagayi aliibuka mshindi akifuatiwa na Bridget Prudence Nakato na Lukia Balunywa, katika nafasi za pili na tatu mtawalia.
Nagayi anaanza ukurasa mpya wa maisha yake akiwa Miss Uganda 2026/27, akitarajiwa kuiwakilisha Uganda kwa heshima, kujiamini na dhamira ya kutimiza malengo yake.
Mrembo huyo kutoka eneo la Masaka, ambaye awali aliwahi kutwaa taji la ulimbwende kati ya wanafunziwa shule za upili yaani Miss Uganda High School mwaka 2024, ni mwanafunzi wa zamani wa Shule ya Upili ya Aga Khan.
Hakuweza kuficha furaha yake alipotangazwa mshindi wa mwaka huu, anapomrithi Trivia Elle Muhoza, aliyekuwa Miss Uganda msimu wa mwaka 2025/26.
Fainali hiyo iliwakutanisha washiriki 22 waliofanikiwa kufika hatua ya mwisho baada ya mchujo uliofanyika kote nchini. Pia, warembo wengine walitawazwa washindi katika vipengele mbalimbali.
Hafla hiyo iliambatana na maadhimisho ya miaka 15 ya wakfu wa Miss Uganda Foundation, taasisi inayoongozwa na Brenda Nanyonjo.