Wahitimu 20 waokolewa baada ya kutekwa nyara Nigeria

Wahitimu hao walitekwa nyara tarehe 1 Oktoba walipokuwa wakisafiri kwenda kushiriki mpango wa kitaifa wa huduma kwa jamii katika majimbo ya Abia na Akwa Ibom, kusini mwa nchi hiyo.

KBC Digital News
2 Min Read
Picha kwa hisani ya Reuters

Kundi la vijana 20 waliotekwa nyara kusini mashariki mwa Nigeria wiki iliyopita wameokolewa, polisi wamesema.

Wahitimu hao walitekwa nyara tarehe 1 Oktoba walipokuwa wakisafiri kwenda kushiriki mpango wa kitaifa wa huduma kwa jamii katika majimbo ya Abia na Akwa Ibom, kusini mwa nchi hiyo.

Walifanikiwa kuokolewa na polisi kwa ushirikiano na vyombo vingine vya usalama.

Msemaji wa polisi, Ani Iniedu, alisema katika taarifa iliyotolewa Jumatano kwamba kundi hilo liliokolewa katika eneo la Amakohia Ubi, jimbo la Imo, baada ya operesheni endelevu ya utafutaji na uokoaji.

Vijana hao kwa sasa wanapatiwa huduma na wamepelekwa kufanyiwa uchunguzi wa afya ili kutathmini hali zao baada ya kuokolewa.

Polisi, jeshi na vyombo vingine vya usalama vilifanya misako katika misitu na maficho yanayoshukiwa kutumiwa na wahalifu kwa kutumia taarifa za kiintelijensia, alisema. Hata hivyo, hakueleza iwapo fidia yoyote ililipwa au kama kuna watu waliokamatwa.

Kundi hilo la vijana lilikuwa linashiriki katika mpango wa National Youth Service Corps (NYSC), ambao ni programu ya lazima ya huduma kwa jamii ya mwaka mmoja kwa wahitimu wengi wa vyuo vikuu nchini Nigeria. Washiriki hupangiwa kuhudumu katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Vijana hao walikuwa wakisafiri katika mabasi mawili kwenye barabara kuu kutoka Ibadan, kusini-magharibi mwa jimbo la Oyo, kuelekea kambi za mafunzo ya awali ya NYSC katika majimbo ya Abia na Akwa Ibom, wakati watu wenye silaha walipoyashambulia mabasi hayo.

Taarifa ya BBC

Share This Article