Freshi Barida! Stevo Simple Boy amezea bunge mate

Anachunguza maeneo bunge ya Kasarani, Lang’ata na Kibra, kabla ya kuamua atakapoanzisha kampeni yake.

Marion Bosire
1 Min Read

Msanii maarufu wa mtindo wa rap nchini Kenya, Stevo Simple Boy, ameamua rasmi kuacha kipaza sauti na kuingia kwenye siasa. 

Ametangaza nia yake ya kuwania ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka ujao wa 2027.

Mwimbaji huyo wa kibao cha’Mihadarati’ ambaye jina lake halisi ni Stephen Otieno Adera, alifichua azma yake ya kisiasa wakati wa mahojiano ya hivi karibuni.

Simple Boy alisema kwa sasa anachunguza maeneo bunge matatu makuu ya uchaguzi katika kaunti ya Nairobi ambayo ni Kasarani, Lang’ata na Kibra, kabla ya kuamua ni wapi atakapoanzisha kampeni yake.

Alisema msukumo wake unatokana na nia ya kushughulikia matatizo ya wananchi mashinani, kuunda nafasi za ajira kwa vijana, na kurekebisha mifumo isiyofanya kazi ipasavyo, kama vile ugawaji wa fedha za kufadhili elimu.

Mwanamuziki huyo alimtaja Mbunge wa Mumias East, Peter Salasya, kama mmoja wa watu waliompa msukumo, akisema kuwa watu wa kawaida wanaweza pia kuleta mabadiliko katika uongozi.

Ingawa bado hajajiunga na chama chochote cha kisiasa, msanii huyo alisema yuko tayari kabisa kuwania kiti hicho kama mgombea huru.

Mashabiki sasa wanasubiri kwa hamu kuona ni eneo gani la kiuchaguzi ambalo msanii huyo atalichagua rasmi, huku akijiandaa kuhama kutoka studio na kuelekea kwenye shughuli za Bunge.

Share This Article