Eritrea na Ethiopia zasitisha uhusiano wa kidiplomasia

Eritrea imekanusha madai ya Ethiopia dhidi yake, ikisema kuwa Ethiopia ndio inawahifadhi, inawapa mafunzo na silaha makundi ya upinzani ya Eritrea ili kuanzisha machafuko.

Tom Mathinji
1 Min Read
Ethiopia na Eritrea zasitisha uhusiano wa kidiplomasia.

Ethiopia na Eritrea zimetangaza kusitisha uhusiano wa kidiplomasia, huku mapigano yakiendelea kaskazini mwa Ethiopia.

Siku ya Alhamisi, Ethiopia ilitangaza inafunga ubalozi wake katika Jiji Kuu la Asmara nchini Eritrea, huku ikiwaagiza maafisa 10 wa kidiplomasia wa Eritrea kuondoka nchini Ethiopia ndani ya saa 48.

Utawala nchini Ethiopia, uliwashutumu maafisa hao kwa kujihusisha na shughuli zinazohatarisha usalama wa kitaifa wa Ethiopia.

Kwa upande wake, Eritrea ilitangaza kuvunja uhusiano wake wa kidiplomasia na Ethiopia, kujibu hatua yake ya kuwafurusha maafisa wake kutoka Addis Ababa.

“Eritrea haina budi ili kuchukua hatua ya kukata uhusiano wa kidiplomasia na Ethiopia,” ilisema taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Eritrea kupitia ukurasa wa X.

Wakati huo huo Eritrea imekanusha madai ya Ethiopia dhidi yake, ikisema kuwa Ethiopia ndio inawahifadhi, inawapa mafunzo na silaha makundi ya upinzani ya Eritrea ili kuanzisha machafuko.

Hayo yanajiri huku mapigano yakiendelea kati ya vikosi vya serikali ya Ethiopia na muungano wa makundi yenye silaha.

Siku ya Jumatano na Alhamisi, milipuko ilisikika Jijini Addis Ababa licha ya serikali ya Ethiopia kupiga marufuku ndege zisizokuwa na rubani kupaa katika Jiji hilo Kuu.

Share This Article