Shirika linalohusika na hakimiliki nchini Kenya, KAMP, limeongeza muda wa kuwasilisha majina ya wanaogombea uchaguzi ujao wa wanachama wa Bodi ya Wakurugenzi hadi Ijumaa, Oktoba 2, 2026, saa 11:00 jioni.
Hatua hiyo inafuatia uamuzi wa hivi karibuni wa Baraza la Hakimiliki katika kesi nambari COPTA/E003/2026 iliyohusisha KAMP dhidi ya mdhibiti wake ambaye ni Bodi ya Hakimiliki ya Kenya, KECOBO.
Kwa mujibu wa KAMP, uamuzi huo ulithibitisha uwezo wa kisheria wa shirika hilo kuendesha shughuli zake za utawala na kuwaelekeza wajumbe halali waliosalia wa Bodi kuitisha Mkutano Mkuu Maalum na kuendesha uchaguzi kwa lengo la kuunda upya Bodi kikamilifu.
Katika taarifa kwa wanachama, KAMP ilisema kuongezwa kwa muda kunalenga kuhakikisha wanachama wote wanaostahili wanapata fursa sawa ya kushiriki katika mchakato wa uchaguzi.
Wanachama wanaotaka kuwania nafasi za Bodi wamehimizwa kujaza fomu zinazohitajika za uteuzi na kuambatanisha na nyaraka zote muhimu kabla ya kuziwasilisha kwa msimamizi wa uchaguzi.
Uchaguzi huo unatarajiwa kuwezesha kuundwa upya kikamilifu kwa Bodi ya KAMP na kuimarisha utawala wa shirika.