Ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta unapozinduliwa leo Jumatano na Rais William Ruto, serikali inalenga kupanua miundombinu ya barabara kwenye bandari ya Lamu, kumarisha shughuli za uchukuzi.
Akizungumza kabla ya kuzinduliwa kwa ujenzi wa kiwanda hicho, Waziri wa Barabara na Uchukuzi Davis Chirchir, alisema serikali iko makini kuongeza uwekezaji ili kuchochea ukuaji wa mfumo wa usafiri wa bandari ya Lamu, Sudan kusini hadi Ethiopia almaarufu (LAPSSET), baada ya kampuni ya Dangote kujitolea kujenga kiwanda hicho cha kusafisha mafuta.
“Tunabuni ramani mpya ambayo haitashughulikia tu mpango wa LAPSSET, lakini eneo nzima la Lamu. Tunaposhuhudia kuzinduliwa kwa ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta cha Dangote, tunafuraha kwa kuwa ramani hiyo imekamilika,” alisema Chirchir.
Kulingana na Waziri huyo, serikali pia inalenga kujenga upya uwanja mdogo wa ndege wa Manda, ili uweze kuhudumia ndege kubwa.
“Tutajega upya uwanja huo wa ndege kikamilifu,” alidokeza Waziri Chirchir.