Watu zaidi ya 80 wameripotiwa kutekwa nyara nchini Nigeria kwenye visa viwili tofauti, wengi wao wakiwa wanawake.
Kulingana na maafisa wa utawala nchini humo, utekaji nyara huo umetekelezwa katika majimbo ya Niger na Zamfara, mwishoni mwa wiki iliyopita, huku makundi yaliyojihami yakiwalenga wakulima wanaoishi katika sehemu za mashinani ambako kuna ukosefu wa usalama.
Katika jimbo la Niger, watu 47 wengi wao wakulima, walitekwa nyara walipokuwa wakivuna njugu kwenye eneo la kijamii la Rimi siku ya Jumamosi.
Vyanzo vya habari nchini humo vilisema, majangili waliokuwa wamejihami walivamia mashamba, kuwazingira wakulima na kuwapeleka eneo lisilojulikana.
Shambulizi tofauti lilitekelezwa siku ya Jumapiki katika jamii ya Yargada, jimbo la Zamfara, ambako wanawake 40 walitekwa nyara.
Wakazi walisema kuwa majangili hao pia walivamia jamii jirani, huku wakiteketeza nyumba na kusababisha wakazi kutoroka makwao.
Mashambulizi hayo ya hivi punde yameibua wasiwasi kuhusu usalama wa wakulima na jamii za mashinani katika majimbo hayo mawili, ambapo mashambulizi na utekaji nyara, yameendelea kuhujumu shughuli za kilimo.