Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, amesema ushirikiano kati ya Kenya na Afrika Kusini, umefanikisha ukuaji wa sekta muhimu hapa nchini.
Akizungumza Jumatatu aliposhiriki mazungumzo na balozi wa Afrika Kusini nchini Kenya Salome Mmola, Mudavadi aliye pia Waziri wa Mambo ya Nje, alidokeza kuwa matunda ya ushirikiano wa nchi hizo mbili yameshuhudiwa kutokana na kuimarika pakubwa kwa sekta za biashara, uwekezaji, usalama, kilimo, utalii na elimu.
“Kenya na Afrika Kusini ni miongoni mwa chumi zinazoongoza barani Afrika. Tunaposhirikiana pamoja, tunafanikisha ukuaji wa fursa kwa raia wetu,” alisema Mudavadi.
Waziri huyo aliongeza kuwa viwango bora vya biashara, ushirikiano wa shughuli za majini, mafunzo ya kiufundi, michezo, utamaduni na kuwawezesha wanawake, yametoa fursa tele miongoni mwa Wakenya, hususan kupitia ujuzi, ajira, biashara na utangamano thabiti kati ya raia wa nchi hizo mbili.
Kulingana na Mudavadi, Kenya inalenga kuimarisha zaidi uhusiano huo na Afrika Kusini, kupitia ushirikiano wa kimkakati, ustawi wa pamoja na maslahi pana ya Afrika.