Msanii wa muziki nchini Tanzania Dudubaya ana kila sababu ya kutabasamu baada ya waandaaji wa tamasha ya miaka 30 ya Bongo Fleva kumlipia faini ya BASATA.
Dudubaya na Mratibu wa tamasha hiyo walipigwa faini ya shilingi milioni 3 pesa za Tanzania kila mmoja ambazo ni sawa na shilingi 147, 000, pesa za Kenya kila mmoja.
Adhabu hiyo ilitolewa na BASATA kutokana na ukiukaji wa maadili kwa upande wa Dudubaya wakati wa tamasha ya miaka 30 ya Bongo Fleva Jijini Arusha, Septemba 19, 2026.
Katika taarifa, Madee ali ambaye ni mmoja wa waratibu wa tamasha hiyo alisema, baada ya kupokea maamuzi ya BASATA, wamekubali kuyatekeleza na kwa haraka kulipa faini iliyotolewa kwao, pamoja na kulipa faini iliyotolewa kwa Msani Dudu Baya.
Waandaaji hao wameihakikishia BASATA pamoja na Wadau wa sanaa Nchini Tanzania kwamba wanaheshimu maamuzi yaliyotolewa na wataendelea kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia taratibu na Sheria zilizowekwa.
Aidha, wameeleza kuwa ushirikiano, uwajibikaji na uzingatiaji wa Sheria ni miongoni mwa misingi muhimu katika kulinda, kukuza na kuendeleza sekta ya sanaa Nchini humo.
“Tunatoa shukrani kwa BASATA na Wadau wote kwa ushirikiano wao, huku tukiahidi kuendelea kushirikiana na mamlaka husika katika kuhakikisha Sekta ya Sanaa inakua na kuendelezwa kwa kuzingatiea misingi ya kisheria na kitaaluma,” alisema Madee.
Awamu ijayo ya tamasha hiyo ya miaka 30 ya muziki wa Bongo Fleva itakuwa Zanzibar Oktoba 17, 2026.